Abiy awashutumu waasi kwa ‘mauaji’ mapya huko Oromia

 


Duru mpya ya mashambulizi dhidi ya makabila madogo magharibi mwa Ethiopia imesababisha wanakijiji "wengi" kuuawa - shambulio la pili kama hilo katika muda wa wiki mbili.


Vijiji vya wakulima vinavyokaliwa na watu wa jamii ya Amhara vililengwa, kulingana na mashahidi ambao wamezungumza na BBC.


Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametaja tukio hilo kuwa la "mauaji" na kuapa "kutokomeza" kundi lenye silaha - Jeshi la Ukombozi la Oromo - ambalo alilaumu kwa ghasia hizo.


Kundi hilo bado halijajibu shutuma hizo.


Mashambulizi hayo yalianza alfajiri siku ya Jumatatu katika wilaya ya Hawa Gelan katika mkoa wa Oromia na kuendelea kwa angalau saa tatu.


Wanaume na wanawake, watoto na wazee waliuawa kiholela, walioshuhudia waliambia BBC.


Nyumba zilichomwa moto na walionusurika wanahifadhiwa misikitini.


Bado hakuna idadi rasmi ya vifo lakini kuna hofu kuwa huenda ikawa juu.


Mashambulizi kama hayo dhidi ya walio wachache karibu wiki mbili zilizopita yalisababisha vifo vya watu 338, kulingana na takwimu rasmi. Wanaharakati walisema takwimu halisi ilikuwa kubwa zaidi.


Ethiopia imeshuhudia kuongezeka kwa ghasia za kikabila katika miaka ya hivi karibuni na inaonekana mambo yanazidi kuwa mabaya.